MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amesema maoni yake ya kutaka
umri wa wagombea urais upunguzwe hayalengi yeye kugombea nafasi hiyo.
“Siwezi kutaka Katiba iandikwe kwa ajili yangu … isionekane kwamba
matakwa ya muda mrefu ya vijana ya kutaka umri wa kugombea urais
kupunguzwa, yanalenga kunipa fursa mimi.
“Mimi ni binadamu, naweza nisiwe na sifa za kuwa Rais, lakini kukawa
na vijana wengine wengi wenye umri chini ya miaka 40 wenye uwezo na
uzalendo wa kutosha kushika usukani wa nchi yetu,” amesema Zitto katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Zitto amesema, anaona, kwamba ni vema yakapatikana mabadiliko ya
vizazi katika uongozi wa nchi ili kukabili changamoto za sasa
zinazokabili Taifa.
“Tunapojiandaa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya, ni vizuri vyombo vya
habari vikajikita kutoa taarifa bila tafsiri au kuwatafsiria maoni
ambayo wananchi na viongozi watakuwa wanatoa kuhusu maudhui ya Katiba
Mpya,” amesema.
Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, amevishutumu
vyombo vya habari vilivyohusisha kauli yake ya kutaka kupunguza umri wa
kugombea urais na yeye kuutaka.
“Mimi nikiwa mwanachama na kiongozi wa chama changu, Chadema,
naelewa na kuheshimu taratibu na kanuni tulizojiwekea za kuomba nafasi
za uongozi, ikiwamo ya urais,” amesema.
Ameongeza kuwa, nafasi ya uongozi ndani ya Chadema haiombwi kwenye
warsha na kwamba iwapo wakati mwafaka utafika na kutokana na matakwa ya
jamii, kikiona apewe jukumu lolote hatasita kutekeleza wajibu huo akiwa
au bila kuwa mgombea.
Amesisitiza, kwamba alichozungumza juzi yalikuwa ni maoni yake na
kwamba muda umefika kwa Taifa kupunguza umri wa kugombea urais, akisema
maoni hayo yanazingatia ukweli, kwamba hakuna sababu zozote za kisayansi
zinazomfanya mtu wa chini ya miaka 40 akose sifa za kuwa Rais.
“Msimamo huu nimekuwa nao tangu zamani nikisoma shule na haujawahi
kubadilika. Hakuna mahala popote katika maoni yangu, niliyotoa jana
(juzi) niliposema nataka umri wa urais upunguzwe ili nipate fursa ya
kugombea urais,” alisema Zitto.
Msimamo wa Zitto unafanana na wa Mbunge wa Bumbuli, January Makamba
(CCM), na waliutoa pamoja juzi katika kongamano la kuelimisha vijana
kuhusu Katiba lililomalizika jana Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment