WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti ikiwemo
mwanamke kumuua mumewe kwa kumpiga na mchi na tukio lingine la mchuuzi
kukanyagwa na gari
wakati akifuatilia fedha zake .
Akielezea tukio la kwanza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Zelothe Stephen alisema
kuwa, Aprili 24, mwaka huu, saa tano usiku katika eneo la Kikuyu
Manispaa ya Dodoma Zacharia Sadala (37), ambaye ni mbeba mizigo aliuawa
kwa kupigwa na mchi kichwani kisha kuchomwa kwa kisu shingoni karibu na
koromeo.
Alisema kuwa marehemu alipigwa na mke wake Jeniffer John (37) ambaye anashikiliwa na Polisi kwa sasa kwa tuhuma za mauaji.
Kamanda Zelothe alisema kuwa, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha mauaji
hayo ni ugomvi wa kifamilia.
Katika tukio la pili, Kamanda Zelothe alisema basi la abiria lenye
namba za usajili T. 627 BBD Leyland Bus, mali ya Kampuni ya Wosia wa
Mama, lilimkanyaga mfanyabiashara John Peter (33), na kusababisha kifo
chake papo hapo.
Kamanda Zelothe alisema kuwa, basi hilo lilikuwa likiendeshwa na
Daud Kilimoka (44), ambaye tayari amekamatwa, lilikuwa likitokea Dodoma
Mjini kuelekea Kijiji
cha Manzase.
Akieleza chanzo cha kifo hicho Kamanda Zelothe alisema kuwa, Peter
baada ya kuuza mzigo wake na akiwa bado hajalipwa fedha alining’inia
mlangoni karibu na dereva ili aweze kumuona mtu aliyemuuzia mzigo wake
na aweze kulipwa fedha zake.
Lakini, dereva aliamua kuondoa gari kwa ghafla na mfanyabiashara
huyo akateleza na kuangukia chini ya uvungu wa gari na kukanyagwa na
tairi.
No comments:
Post a Comment