Thursday, May 17, 2012

40 ya Kanumba Giza latanda!!!


Marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’.
Mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa.
Baba mzazi wa marehemu Kanumba, Mzee Charles Kanumba.…
Marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’.
Mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa.
Baba mzazi wa marehemu Kanumba, Mzee Charles Kanumba.
Sehemu ya umati uliohudhuria msiba wa marehemu Kanumba.
Issa Mnally na Shakoor Jongo
LEO ni siku ya arobaini tangu kifo cha aliyekuwa nyota wa sinema za Bongo, Steven Charles Kanumba ‘The Great’ lakini giza nene linaonekana kuigubika shughuli hiyo kufuatia tamko la mama wa marehemu, Amani linakuja na habari kamili.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu juzi Jumanne, mama wa marehemu, Flora Mtegoa alisema ni kweli arobaini imefika lakini hajui kinachoendelea ila itafanyika Mei 20, 2012.
TAMKO LA MAMA
Mama Kanumba alikuwa akijibu swali la kipaparazi lililomtaka afafanue kama mkusanyiko wa arobaini ya marehemu utakuwepo au kila mtu atakuwa kivyake.
“Nimeambiwa itafanyika tarehe 20 mwezi huu lakini zaidi ya hapo sijui chochote kile kinachoendelea mwanangu,” alisema mama huyo kwa sauti iliyojaa unyenyekevu.
HABARI NDANI YA TASNIA YA SINEMA
Amani lilizungumza pia na mmoja wa wasanii wa filamu za Kibongo ambaye hakupenda jina lake liwekwe wazi. Yeye alikuwa na haya ya kusema:
“Ilibidi arobaini yake
ifanyike Mei 17 (leo) lakini kila tukiulizia tunaambiwa mipango bado haijakamilika, mipango gani hiyo kama fedha zilipatikana nyingi sana katika rambirambi.
“Wanaona hasara kuzitoa kwa ajili ya kununulia vifaa vya arobaini?”
Aidha, msanii huyo aliitaka kamati ya maandalizi ya arobaini hiyo (kama ipo) kutoifanya kienyeji na kushauri kuwa inabidi itangazwe ili watu wahudhurie kwa wingi kama siku ya mazishi.
“Kinachoonekana wanataka kufanya shughuli bora ifanyike, watakuwa wameharibu sana. Wakifanya shughuli kubwa pengine hata rais au mawaziri na wabunge wanaweza kuhudhuria,” alisema msanii huyo.
MANENO YA JB
Msanii Jacob Steven JB, Mwenyekiti wa Bongo Movie, alipoulizwa na gazeti hili siku ya Jumanne (juzi) alisema hajui lolote kuhusu arobaini hiyo.
Akasema: “Kwa taarifa nzuri labda muulize Gabriel Mtitu ‘Mtitu Game’ (aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maziko), yeye atakuwa anajua lolote.”
SAUTI YA MTITU GAME
Amani lilimtwangia simu Mtitu Game na kumuuliza kama anajua lolote kuhusu kuwepo kwa arobaini ya marehemu Kanumba.
“Aaa, yeah! Arobaini imeangukia Alhamisi, siku ya kazi. Kwa hiyo familia ikaona ifanyike Mei 20, mwaka huu ambayo itakuwa Jumapili,” alisema Mtitu.
Amani: “Kwa hiyo ishu itakuwaje?”
Mtitu: “Aaa! Kutakuwa na ibada pale Kanisa la AIC Chang’ombe, halafu baadaye wanandugu watakusanyika nyumbani kwa marehemu (Sinza) kwa ajili ya chakula cha pamoja.”
Amani: “Hakuna mwito kwa mtu yeyote atakayetaka kuja?”
Mtitu: “Sijalijua hilo.”
BABA KANUMBA NAYE
Baada ya mawasiliano yote hayo, Amani lilimpigia simu baba mzazi wa marehemu, Mzee Charles Kanumba na kumuuliza kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa arobaini ya mwanaye.
Akafunguka: “Sijajua, ila lazima iwepo.”
Amani: “Huku mama wa marehemu naye anasema hajui lolote, wewe unasema hujajua.”
Baba: “Yeye (mama Kanumba) kusema hajui lolote ni janja ya nyani tu. Mimi najiandaa kuja huko siku mbili hizi, nikifika kila kitu kitajulikana.”
CHANZO CHA YOTE
Chanzo cha yote haya ni simu zilizoanza kumiminika kwenye Ofisi za Global Publishers, wasomaji wa Dar na mikoani wakiulizia shughuli hiyo itafanyikia wapi ili wahudhurie.
Juma Makala wa Mwanza, alitaka kujua siku na mahali ili aweze kufika baada ya kushindwa kuhudhuria mazishi ya marehemu.
“Jamani naitwa Juma Makala, niko Mwanza. Hivi hii arobaini ya Kanumba ni lini? Nahisi imekaribia. Na itakuwa wapi? Kwa sababu sikuweza kuhudhuria kwenye mazishi sasa nilitaka kujua ili niweze kufika.”
Amani lilimjibu aendelee kufuatilia magazeti ya Global atajua ni lini.
Mama Mage wa Kinyerezi, Dar yeye alisema alitaka kwenda Afrika Kusini kwa matibabu lakini amesitisha kusubiri arobaini ya Kanumba lakini hajui itakuwa lini.
Amani lilimuomba kuendelea kusoma magazeti ya Kampuni ya Global Publishers ili kujua ni lini na wapi.
NENO LA MHARIRI
Arobaini ya Kanumba imefika, kama ni Mei 20 ni vyema watu wakasubiri tamko maalum la familia ambalo naamini litaweka wazi hata wenye sifa za kuhudhuria.

No comments: