Saturday, June 30, 2012

Pinda: Tunachunguza bilioni 300 za Uswisi



 WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali kupitia vyombo vyake vya dola, imeanza kuchunguza taarifa za kuwapo kwa Sh300 bilioni zilizofichwa nchini Uswisi.Pinda aliliambia Bunge jana kuwa, Serikali pia ilisoma taarifa kwenye vyombo vya habari kama walivyosoma wabunge, na kwamba tayari wameanza uchunguzi kuhusu suala hilo na baada ya uchunguzi matokeo yatatangazwa.

Alivitaja vyombo vinavyochunguza tuhuma hizo kuwa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Kuchunguza na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kitengo cha Kiiteliejensia cha Wizara ya Fedha (Fiu).

Pinda aliyasema hayo jana wakati akijibu hoja za baadhi ya wabunge, ambao katika kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu walitaka kupewa maelezo ya kutoroshwa kwa fedha hizo.

Taarifa za kufichwa kwa fedha hizo kwenye akaunti sita za wanasiasa na vigogo wa Serikali, ziliripotiwa wiki iliyopita na magazeti ya Mwananchi na The Citizen pekee, zikinukuu ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB), iliyotolewa hivi karibuni, ikitaja nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, na kiwango cha fedha zilizohifadhiwa huko.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine ambazo zina fedha nyingi katika benki za Uswisi ni Kenya (Dola 857 milioni), Uganda (Dola 159 milioni), Rwanda (Dola 29.7 milioni) na Burundi Dola 16.7 milioni.

Chanzo cha habari hizo kilieleza kuwa, tangu akaunti hizo zifunguliwe na kampuni za kuchimba mafuta na madini, wamiliki wake halali kutoka hapa nchini, hawajawahi kuingiza hata shilingi moja.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akichangia bajeti ya Waziri Mkuu, aliitaka Serikali kuchunguza, kuwataja na kuwachukulia hatua wamiliki wa akaunti hizo.
 
Alisema, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ielekezwe ili ifanye uchunguzi utakaowezesha wamiliki wa akaunti zao kufahamika ili wachukuliwe hatua mara moja bila kujali nafasi wanazozishika serikalini.

Jana akijibu hoja za wabunge, Pinda alisema: “Serikali kupitia vyombo vyake (Takukuru, Financial Intelligency Unit (Fiu) wameanza kufanya uchunguzi wa taarifa hizo kwa kuzingatia taratibu za kisheria.”

Pinda pia alionya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali, unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Serikali wasio waaminifu wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Kwa kweli hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hiyo, na sisi tunasema wabunge kupitia kamati zetu zile tatu za masuala ya fedha na kamati nyingine za kisekta mnatusaidia sana maana lazima tubadilike ili tuweze kutoka hapa tulipo,”alisema Pinda.

Pinda alisema Serikali haijalifumbia macho suala hilo na kwamba hatua stahiki za kinidhamu zimekuwa zikichukuliwa kwa viongozi na watendaji wa aina hiyo kila walipobainika.

“Mathalan katika kipindi cha mwaka 2011/2012 wakurugenzi wapatao 48 walichukuliwa hatua za kinidhamu au kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu ikiwa ni pamoja na vitendo vya wizi, rushwa, ubadhirifu, ukiukaji wa maadili na kushindwa kutekeleza majukumu yao,” alisema Pinda.
Pinda pia alizungumzia kwa undani mgawanyo wa fedha za rada zilizorejeshwa kutoka Uingereza, maarufu kama chenji ya rada, kuwa zitatumika kwa ununuzi wa vitabu na madawati, kwa kuwa ndiyo makubaliano yaliyofikiwa na pande husika.

Pande hizo ni Serikali kupitia Wizara ya Fedha, wakati Uingereza iliwakilishwa na DFID, BAE Systems na SFO.

“Matumizi ya fedha hizo yanalenga kuimarisha uendeshaji wa Elimu ya Msingi ambapo asilimia 75 ya fedha zitatumika kununua vitabu vya kiada, vitabu vya mwongozo kwa walimu, mihutasari na miongozo ya mihutasari, asilimia 25 itatumika kununua madawati,” alisema Pinda.
Alisema vitabu hivyo vitanunuliwa kutoka kampuni 13 za wachapishaji zilizoteuliwa ambazo, ni Ben Company, Best Deal Publisher, E & D Vision, Education Books Publisher, Jadida, LongHorn, Longman, Macmillan, Mkuki na Nyota, Mture, Oxford, Taasisi ya Elimu Tanzania na Ujuzi Book.

Pinda aliongeza kuwa kati ya kampuni hizo, kinyume na ilivyodaiwa na baadhi ya wabunge, mbili tu ndiyo za nje, lakini zina matawi hapa nchini na kwamba kampuni nyingine zilizobaki wamiliki wake ni Watanzania.

Daktari: Hali ya Ulimboka mbaya


Mgonjwa akiwa nje ya geti la Taasisi ya Mifupa MOI jijini Dar es Salaam jana akiwa ajui chakufanya baada kukuta geti hilo limefungwa kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.Picha na Venance Nestory
ASEMA FIGO ZAKE ZIMESHINDWA KAZI, ZATAKIWA DOLA 40,000 KUMPELEKA INDIA
Geofrey Nyang’oro na James Magai
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka imebadilika na kuwa mbaya, baada ya figo zake kushindwa kufanya kazi ya kuchuja sumu ya mwili na kusababisha apatiwe huduma ya kusafisha damu yake.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na kiongozi wa jopo la madaktari wanaoendelea kumtibu, Profesa Joseph Kahamba, zilieleza kuwa hali ya Dk Ulimboka ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo kuwapo mikakati wa madaktari wenzake kukusanya fedha ili kumpeleka nje ya nchi.

Dk Ulimboka ambaye amelazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alipatiwa huduma hiyo jana asubuhi kwa kutumia mashine maalumu, iliyoko katika Kitengo cha Watoto cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Daktari huyo ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, amelazwa kutokana na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha, meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano.

Tangu alazwe MOI baada ya kuokotwa na wasamalia wema, katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dares Salaam, hali ya afya ya Dk Ulimboka imekuwa tete na jana ilizidi kuwa mbaya.

Kauli ya Dk Kahamba

Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Kahamba alisema kutokana na tatizo hilo, mgonjwa huyo jana alilazimika kusafishwa damu.

Alieleza hayo alipotakiwa kuthibitisha taarifa zilizolifikia gazeti hili kuwa afya ya Dk Ulimboka haikuwa nzuri na madaktari wanachangishana fedha kumpeleka kwenye matatibu ya kusafishwa damu katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam au nje ya nchi.

"Taarifa hizo zina ukweli, lakini siyo jambo rahisi kiasi hicho kwamba anatakiwa kusafishwa damu. Kama ni damu amesafishwa leo (jana) asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili," alisema Profesa Kahamba na kuendelea:

"Suala lake ni complicated (tata) zaidi, lakini ili watu waelewe, siyo mbaya mkisema figo zimefeli(zimeshindwa kufanya kazi)."

Alipotakiwa kueleza sababu ya tatizo hilo, Profesa Kahamba alisema, "Siwezi kueleza kwa undani ila haya maumivu ya kupigwa na kuteswa yanachangia kwa kiasi kikubwa."

Alipotakiwa kueleza yeye anaonaje hali ya sasa ya Dk Ulimboka, Profesa Kahamba alisema: “Ni uongo tukisema anaendelea vizuri."

Aliendelea, "Unajua alipofikishwa hapa Muhimbili juzi (Jumatano) afya yake ilikuwa mbaya, na jana (Alhamisi) alionekana kuendelea vizuri, lakini jana hiyohiyo, hali yake ilianza kubadilika na vipimo vilionyesha kuwa ana complications (matatizo) za figo.

"Sasa figo ni kitu sensitive (muhimu) sana, anahitaji uangalizi wa karibu na kimsingi hatuwezi kusema kwamba anaendelea vizuri. Ni vyema tukisema tu afya yake ni mbaya," alieleza.

Taarifa za awali kutoka kwenye chanzo chetu hospitalini hapo, zilieleza kuwa Dk Ulimboka ambaye alipata tatizo linalojulikana kama “Acute renal failure”, alifanyiwa tiba inayojulikana kama Dialysis, ambayo ni kitendo kutumia mashine maalumu kufanya kazi ya kuchuja sumu ya mwili kwenda kwenye mkojo, baada ya figo ambazo hufanya kazi hiyo kushindwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Dialysis inaweza kumsadia mgonjwa ambaye figo zake zimeshindwa kufanya kazi, kuishi kama kawaida, lakini kwa Dk Ulimboka haikutoa matokeo mazuri.

Michango ya madaktari

Jana ulifanyika Mkutano wa Madaktari Bingwa wa MNH, Chuo Kikuu Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ocean Road (ORCI) na kuazimia kukusanya Dola za Marekani 40,000 (Sh64,000,000) ili Dk Ulimboka asafirishwe kwenda India kwa matibabu zaidi.

Taarifa za maazimio hayo zilitangazwa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitega, kuwa afya ya Dk Ulimboka haikuwa nzuri hivyo zikipatikana fedha hizo angepelekwa nje ya nchi.

Dk Chitega aliwataka wanataaluma hao na wananchi kwa ujumla kuchangia safari hiyo ili kuokoa maisha ya daktari huyo, huku akitaja namba za mawakala wa simu za Vodacom na Tigo, ambazo zitatumika kukusanya michango hiyo.

Habari zilizopatikana baadaye wakati tunakwenda mitamboni zilieleza kuwa, Dk Ulimboka alitarajiwa kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.


TANNA MOI watoa tamko
Katika hatua nyingine, Chama cha Wauguzi (Tanna), Tawi la MOI kilitoa tamko la kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka na kutaka uchunguzi wa kina na haraka ufanyike ili kubaini watu waliohusika.

Mwenyekiti wa Tanna, Tawi la Moi, Prisca Tarimo alisema katika tamko hilo kuwa, kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kisicho cha kiutu.

Katika tamko hilo, Tanna imeomba Serikali kutafuta suluhu ya mgomo huo haraka kwa kuwa unaathiri maisha ya watu na kuwaongezea mzigo wa kiutendaji wauguzi.

Mgomo wa madakati unaingia siku ya saba leo, huku suluhu ya kuaminika ya kutatua tatizo hilo, ikiwa bado haijapatikana.

Polisi wakanusha
Katika hatua nyingine, James Magai anaripoti kuwa, Jeshi la Polisi limekanusha kumteka na kumjeruhi Dk Ulimboka, huku likipinga pia taarifa za daktari huyo kumtambua mmoja wa askari walio katika jopo la uchunguzi wa tukilo hilo alipokwenda kumtembelea hospitalini.

Pia jeshi hilo limetoa wito kwa madaktari hao walioko katika mgomo kuwa na busara na kutii amri ya Mahakama, ya kuwataka wasitishe mgomo wao.

Pia limeonya kuwa ikiwa wataendelea kukaidi na kupuuza amri ya hiyo ya mahakama, linao wajibu wa kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha mahakamani, ili wajibu mashtaka hayo.

Msimamo huo ulitolewa jana na Kamishna wa Oparesheni Maalumu, Kamishna wa Polisi (CP), Paul Chagonja wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano alioitisha kuzungumzia matokeo ya operesheni ya jeshi hilo ya majuma matatu katika kuzuia uhalifu nchini.

Alisema madai hayo ni uvumi ambao unalenga kulifanya jeshi hilo lisiaminike na kufifisha juhudi zake za kuwasaka waliohusika na unyama huo.